HII NDIO SHULE ILIYOSHIKA NAFASI YA MWISHO KITAIFA KATIKA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE
MATOKEO ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yaliyotangazwa
mwanzoni mwa juma, yanaendelea kutawala mijadala mbalimbali kila kona.
Sababu kubwa ya mijadala hiyo kutawala yaweza kuwa ni
takriban kila familia kuguswa kwa njia moja ama nyingine na matokeo hayo.
Katika matokeo hayo karibu shule zote za umma zimefanya vibaya, zile za
kata zikiongoza katika kufelisha, huku ile ya Mibuyuni iliyopo Kilwa
mkoani Lindi ikiwa ya mwisho kabisa katika kundi la shule zenye zaidi ya
wanafunzi 40.
Mkuu msaidizi wa shule hiyo Robart Mzumbi,
alisema kuwa matokeo hayo yalitarajiwa kwa kuwa tangu wanafunzi hao
walipoandikishwa kidato cha kwanza, hawakuwa wamefaulu.
Alibainisha kuwa, matokeo ya kidato cha pili ya wanafunzi hao
walipofanya mtihani wa taifa mwaka 2010, yalikuwa kiashiria kingine
kwamba, hata kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wanafunzi hao
hawatafanya vizuri.
Pamoja na hayo, Mzumbi anaeleza kwamba kwa
kuwa lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha wanafundisha watoto hao na
mwisho wafanye vyema, matokeo hayo yamewasikitisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaja upungufu wa walimu na umaskini wa kipato kwa jamii
inayozunguka shule hiyo kuwa ni moja ya sababu kubwa zilizosababisha
matokeo hayo mabaya.
Mwalimu huyo alibainisha kwamba
idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hujishughulisha
zaidi na biashara ndogo ndogo, badala ya kusoma.
Aliweka wazi
kuwa, shule hiyo ilikuwa ya mwisho kati ya shule 3,392 zenye watahiniwa
40 na kuendelea, wakati watahiniwa hao wa mwaka 2012 walipochaguliwa
kuingia kidato cha kwanza mwaka 2009, ambapo walikuwa na alama za chini.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao walichaguliwa kuanza kidato cha
kwanza wakati tayari wengi wao walishaanza kufanya biashara ndogondogo,
hivyo walikusanywa kutoka huko mitaani na kupelekwa shule.
“Ndugu yangu shule yetu huwa inafanya vizuri kidogo, angalia matokeo ya
kidato cha pili mwaka huu Sekondari ya Mibuyuni imekuwa ya 115 kati ya
shule 242 za Kanda ya Kusini, wanafunzi wanane wamefaulu kati ya 25
waliofanya mtihani. Lakini kwa matokeo ya kidato cha nne, kwa kweli
wanafunzi waliochaguliwa mwaka 2009, hawakuwa na sifa bali waliokotwa tu
ili kujaza darasa,” alisema na kuongeza:
“Hata mtihani wa kidato cha pili mwaka 2010, walifanya vibaya sana na shule hii ilikuwa ya pili kutoka mwisho.”
Mzumbi alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwamo kukosa maabara, upungufu wa walimu wa sayansi, usafiri na umeme
wa uhakika.
Pia ina ukosefu wa maji, nyumba za walimu, mabweni
kwa ajili ya watoto wa kike, pamoja na shule kujengwa mbali na makazi
ya wananchi.
Alieleza kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika
shule mbalimbali za Mkoa wa Lindi, hulazimika kutembea umbali mrefu
kutoka nyumbani kwenda shuleni.
source:mwananchi.co.tz